Hongera Rais Samia kusimamia bima ya afya kwa watu wote tulichelewa wapi?

Share on facebook
Share on twitter
Share on linkedin
Share on whatsapp
Share on print

Dar Es Salaam. May 3, 2021. Mch. Dkt. Peter Bujari


March 2019 nilimwandikia barua ya wazi (kupitia gazeti la Mwananchi) Raisi wa Tanzania wakati huo Hayati John Pombe Magufuri kumshauri kuichukua agenda ya huduma za afya kwa wote na kuwahimiza wasaidizi wake kuisimamia. Bahati mbaya halikupata 

kipaumbele.

Raisi wa sasa ameelekeza wizara husika kuhakikisha linafanyika. Nimelazimika leo kuandika Makala hii kufufua agenda hii na kutoa mapendekezo ya kitaalamu na ya namna ya kuendelea.

Septemba mwaka 2015 Umoja wa mataifa katika mji mkuu wa Marekani New York ulipitisha azimio la maendeleo endelevu la kiafya (SDG 3) na lengo la nane (SDG 3.8) lilikuwa kufikia afya kwa wote ifikapo mwaka 2030. Dhana ya upatikanaji wa huduma ya afya kwa wote umejengwa kwenye msingi wa usawa na haki za binadamu (Kifungu cha 25),  hivyo utekelezaji huo utaharakisha kufikia malengo mengine pia.

 Septemba 23rd mwaka 2019, umoja wa mataifa ulifanya kikao rasmi kujadili maendeleo na uwekezaji katika afya kwa wote, nchi nyingi zilionekana kusuasua, ikiwemo Tanzania. Shirika la afya duniani liliripoti kuwa angalau mtu mmoja kati ya kumi hapa Tanzania hutumia karibu asilimia kumi ya kipato chake kwa mwaka kwa ajili ya huduma za afya. Ushahidi wa kitaalamu kutoka chuo kikuu cha Imperial College cha London unaonyesha kuwa kuwekeza kwenye afya kwa wote huboresha afya ya jamii na matokeo makubwa yakionekana kati ya watu masikini Zaidi, vifo vya Watoto wachanga vikipungua na wastani wa umri ukiongezeka. Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Afya kwenye hotuba yake ya mwaka 2018/19 kifungu namba 118 ilisema serikali inalenga kufikia mwaka 2020 Watanzania asilimia 70 wawe na bima ya afya. Mpaka mwaka jana ni asilimia 34 tu walikuwa na bima ya afya. Ili kufikia lengo hilo, serikali ilitakiwa kupitisha mkakati wa kifedha wa kugharimia huduma za afya (Health Financing Strategy), kuwa na mfumo wa kutoa ruzuku ya bima kwa watu wa hali ya chini (subsidized insurance), Kuwa na sera na sheria jumuishi (Social participation). Kwa bahati mbaya, haya hayakufanyika, hivyo kufanya uwezekano wa lengo hilo kuwa mdogo. Kwa vile Raisi ameelekeza mchakato huu uanze tena, hayo ni mambo muhimu kuzingatia. Hatua ya Raisi kuelekeza bima ya afya kwa wote inamaanisha yafuatayo: (a) Kutangaza kuwa kusiwepo na Mtanzania anayekosa huduma za afya kwa kutokuwa na hela, (b) Kupitisha mpango mahususi wa mfumo utakaotumika kuhakikisha watu wa hali ya chini wanakuwa na bima ya afya, (c) Kupitisha na kutekeleza mkakati wa kugharimia huduma za afya (National Health Financing Strategy) na (d) Kuweka malengo ya kuongeza matumizi kwenye sekta ya afya kufikia asilimia 4-5 ya pato la taifa kutoka kwenye 1.7% ya mwaka 2016 kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani na (e) Kujenga na kuhakikisha zahanati zinazotoa huduma zinaongezeka kutoka 43 ya sasa kwenye vijiji mpaka angalau 75%. Ikiwa Raisi Samia akisimamia hili kwa ufanisi, atakumbukwa na watanzania wengi na kupata umaarufu wa kisiasa kama Tommy Douglas waziri mkuu wa Canada ambaye aliitwa Shujaa wa Mageuzi ya Afya kwa Wote mwaka 2004. Raisi wa China Hu Jintao mwaka 2006 alibeba agenda ya afya kwa wote akafikia 95 ya wachina wote na hivyo wananchi kuwekeza kwenye maendeleo kitu ambacho Pamoja na mambo mengine kimeifanya China kuwa nchi ya pili kwa uchumi imara duniani. 

Wasiliana nasi. successadvisor@peterbujari.com 

15 thoughts on “Hongera Rais Samia kusimamia bima ya afya kwa watu wote tulichelewa wapi?”

  1. Leonard Kabogo

    Mh Mwandishi nakupongeza sana kwa wito wako na kuonyesha msisitizo wa kutaka jambo ili jema liwe faida kwa kila mtanzania

  2. Razius Banobi

    Nami pia nichukue nafasi kwanza kukupongeza wewe mwandishi Dr Peter Bujari kwa kazi yako njema zaidi niungane kumpongeza rais kuliekeza jicho lake kwenye hii sekta muhimu ya afya watanzania wito wangu tushirikiane na serikali yetu kulifanikisha swala hili

  3. Norbert Seleman

    Ndugu Peter Bujari Daktari Hongera sana kwa hatua hii kubwa uliyoifikia katika kupigania masilahi ya watu wote hakika nyazo zako zinapaswa kufuatwa kwa nafasi hii niseme tu kwamba ikiwa watu kama nyie mtaendelea kuzungumza na kuishauri serikali basi tuelekeako ni kuzuri sisi tuko tayari kuwaunga mkono kwa kila jema mnalo lifanya na ni muhimu kujua kua watanzania na dunia nzima inahitaji watu kama wewe ili kufanikisha mambo makubwa.

  4. Mwal Athumani Jamal

    Andiko lako ni kubwa na wenye marifa na uzalendo wamekuelewa tuendelee kuwasemea wananchi wetu

  5. Anna Dominick

    Mimi ni Mmoja wa wadau katika sekta hii ya afya naunga mkono upatikanaji wa bima ukizingatia kuwa asilimia ya watu wanatumia pesa nyingi katika kutafuta huduma za afya na kwa sababu hiyo uchumi wa watunbinafsi una shuka, tuna safari ya kulisisitiza hili kwa pamoja.

  6. Peter Bujari MD

    Mdugu wapendwa Anna, Mwl Arhumani, Norbert, Razius na Leonard
    Asanteni kwa pongezi. Naamini kuwa raisi ana nia thabiti juu ya hili na mengine. Tumuunge mkono.

  7. Mimi ni mtanzania ninayeishi New York hapa Amerika, ni mzalendo wa taifa langu na mdau mkubwa wa maendeleo. Nimeona furaha sana kukutana na Article hii na kwa undani nimengundua umelenga kuzungumza hasa kwenye maswala yenye tija kwa kila mwananchi, na mimi pia niungane na wengine kukupongeza kwa hatua hii kubwa lakini zaidi kwa niaba ya watanzania wote waishio Marekani tukuhakikishie kuwa sisi wadau tuko pamoja na wewe katika kuhakikisha tunaunga mkono juhudi za kufanikisha mipango mikubwa na endelevu kama hii.

    1. Bwana Dastan. Nakushukuru sana. Ni lengo langu kutoa mchango wangu kwa viongozi wetu kuthamini wananchi na kutengeneza maziingira ambayo wananchi wanajisikia kuipenda serikali yao. Ni kwa sababu hii ninaanzisha mafunzo ya uongozi wenye tija ( High Impact Leadership). https://peterbujari.com/instute/. Karibu tushirikiane kuisogeza nchi yetu mbele

  8. Mimi ni muhudumu wa afya na nina shuhuda za maumivu wanayo yapitia wananchi wasio na bima za afya, kupitia ujumbe huu Nafikiri ni wakati wa viongozi wetu kufikia hatua ya kuelewa na kufanya vitu vyenye faida kwa watanzania wote.

  9. Nakuunga mkono Dr.Bujari;
    Watakubaliana nami watu tunaofanyakazi katika sekta ya afya hususani ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya; Pamoja na wizara ya afya kuongeza bajeti katika wizara ya afya kuanzia mwaka 2016 bila kupepesa macho bajeti hiyo mwananchi wa chini haijamfikia na kunufaika nayo. Tumeshuhudia kuzorota kwa huduma za afya zilizopelekea matibabu kuwa ghali sana nchini, tumeshuhudia vituo kupitia mazingira magumu ya kukosa hela za kuendeshea vituo hivyo, tunashuhudia mpaka sasa kukosekana kwa miundo mbinu ya mawasiliano ya kihuduma hasa mgonjwa anapotoka ngazi moja kwenda nyingine kwaajili ya matibabu mathalani mgonjwa anayetibiwa kwa CHF katika zahanati au kituo cha afya, anapopewa rufaa kwenda hospitali hasa za mikoa na rufaa bima yake ya CHF inakuwa haina thamani tena mgonjwa huyo hulazimika kulipia matibabu kwa hela yake ya mfukoni hili ni la ukweli sio uzushi. Wanawake wajawazito tunaofanyia rufaa, wakifika hospitali wanalazimika kulipia huduma zinazohusu upasuaji kama vile kununua gloves, drips na gharama za surgery hili ni la ukweli sio uzushi. Kumbuka mzazi huyo amekodi gari ameweka mafuta kumsafirisha kwenda hospitali kutokana na baadhi ya vituo tulivyopo kukosa usafiri, kukosa mafuta na mambo mengine. Hapo nimeaangazia baadhi tu ya maeneo ambayo mwananchi wa kawaida anapata shida ambazo nazishuhudia nami nikiwa mhanga wa kupambana nazo. Naamini tunashida kubwa kuliko hizi. Ni wakati muafaka nchi inapofikia hatua ya uchumi wa kati basi ujinasibu katika huduma za kijamii kama hizo. Bima ya afya kwa wote ndio Suluhu. na hiyo iCHF iangaliwe upya bado haikidhi mahitaji ya kuleta huduma endelevu. Mfano mgonjwa katibiwa matiba ya thamani ya elfu 50, kituo kinalipwa hela ndogo saaana.

    1. Asante Vasco. Tunapata ushahidi wa hali halisi ilivyo. Mtu mmoja ameniambia kuwa alilipia bima, baadae akaacha. NIkamuuliza kwanini aliacha, akasema kila alipoenda kituoni hakukuwa na dawa. Hivyo aliacha maana hakuona haja. Tunahitaji mabadiliko

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *